Wizara Ya Afya

DAWA, VIFAA TIBA KUFIKIA UZALISHAJI WA ASILIMIA 60, IFIKAPO 2030

Posted on: July 1st, 2026


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema Serikali imejipanga kuhakikisha Tanzania inafikia utoshelevu wa dawa na vifaa tiba kwa zaidi ya asilimia 60 ifikapo mwaka 2030 kupitia uwekezaji wa viwanda vya ndani vinavyozalisha bidhaa za Afya.

Rais Dkt. Samia amesema hayo leo, Julai Mosi, 2026, Ikulu jijini Dar es Salaam, wakati wa hafla ya kumuapisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dkt. Grace Magembe.

Rais Samia amemtaka Dkt. Magembe kutumia kwa ufanisi bajeti ya mwaka wa fedha 2026/27 iliyopitishwa na Bunge hivi karibuni ili kuharakisha utekelezaji wa vipaumbele vya sekta ya afya vinafikiwa.

“Nendeni mkakaribishe wawekezaji wa viwanda vya dawa na vifaa tiba waje kuwekeza Tanzania, lakini zingatieni viwango vya ubora. Kalifanyieni hili kazi kwa umakini,” amesema Rais Dkt. Samia.

Amesema uwekezaji katika viwanda vya ndani utaiwezesha Tanzania kuongeza upatikanaji wa dawa na chanjo, ikiwemo chanjo za watoto na magonjwa mengine, hatua ambayo itapunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje, kuokoa fedha za kigeni na kuhakikisha bidhaa hizo zinapatikana kwa haraka na kwa urahisi zaidi.

Rais Dkt. Samia pia amemtaka Dkt. Magembe kujenga ushirikiano mzuri na watumishi wa sekta ya afya ili kuendelea kuboresha huduma za afya kwa Watanzania.

“Wewe ni Daktari; nenda ukafanye kazi na madaktari wenzako. Madaktari wakikukataa hutaweza kufanya kazi. Kazi niliyokupa ni ya utawala na usimamizi. Ingawa wewe ni Daktari, uzoefu ulioupata ulipokuwa Naibu Katibu Mkuu TAMISEMI na badae ukiwa Mganga Mkuu wa Serikali na katika nafasi nyingine mbalimbali, unanipa imani kuwa utaimudu kazi hii,” amesema Rais Dkt. Samia.

Dkt. Grace Magembe ameapishwa kufuatia uteuzi wake wa hivi karibuni kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya akichukua nafasi ya Dkt. Seif Shekalaghe aliyeteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, kabla ya uteuzi huo Dkt. Magembe alikuwa ni Mganga Mkuu wa Serikali.