DAR ES SALAAM YAIMARISHA TIMU ZA RCCE KUKABILIANA NA EBOLA NA ATHARI ZA EL NIÑO
Posted on: October 7th, 2026Na Atley Kuni, WAF-Dar es Salaam
Mkoa wa Dar es Salaam umeendelea kuimarisha utayari wa timu za Mawasiliano ya Hatari na Ushirikishwaji wa Jamii (RCCE) katika Halmashauri za Kigamboni, Temeke na Ubungo, ikiwa ni sehemu ya zoezi la kitaifa linalotekelezwa kwenye mikoa 12 chini ya Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu–TAMISEMI pamoja na wadau, kwa lengo la kuziwezesha Halmashauri kuwa tayari kukabiliana na tishio la Ebola pamoja na athari zinazoweza kujitokeza kutokana na mvua za El Niño.
Akitoa tathmini ya jumla mara baada yakupitia Dodoso kwa mkoa huo Oktoba 7, 2026 mratibu kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI Chipole Mpelemba amesema kwa Wilaya ya Kigamboni, timu imejikita kuimarisha utoaji wa taarifa za tahadhari kwa jamii, kutambua maeneo yaliyo katika hatari ya mafuriko na kuhamasisha wananchi kuchukua hatua za kinga mapema.
Kwa upande wa Wilaya ya Temeke yenye wakazi zaidi ya milioni 1.3, kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, Mpelembe amesema maandalizi yamejikita kuimarisha uratibu wa wataalamu wa afya, viongozi wa Halmashauri na jamii, huku elimu ikilenga utambuzi wa dalili, utoaji wa taarifa mapema, kinga dhidi ya magonjwa ya mlipuko na hatua za kuchukua wakati wa mvua kubwa.
Kwa Manispaa ya Ubungo amesema imeendelea kuimarisha utayari kwa kutambua maeneo yanayoweza kuathiriwa na mvua kubwa, pamoja na kuhamasisha ushiriki wa wananchi kwa usafi wa mazingira na uondoaji wa vikwazo kwenye mifereji na mito.
Mratibu huyo kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu–TAMISEMI, awali alitoa wito kwa mikoa ya Iringa na Ruvuma akisisitiza kuwa maandalizi yanapaswa kufanyika wakati hali ikiwa shwari ili kupunguza athari wakati dharura inapotokea.
"Rai yangu nikuona mnatumia taarifa zinazokusanywa kutoka kwa jamii kupanga elimu inayolenga mahitaji halisi ya wananchi, huku mzingatia pia makundi maalum kama watoto wa shule", amesema Mpelembe.