CHANJO HUIMARISHA KINGA YA MWILI KWA WATOTO
Posted on: March 25th, 2026Na Hassan Kimweri, WAF - Mwanza
Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Grace Magembe amesema chanjo huimarisha kinga ya mwili kwa watoto ambayo kwa sasa itatolewa katika mikoa Saba na timu zaidi ya elfu kumi na nne (14,000) zitatoa huduma hizo.
Dkt. Magembe amesena hayo leo Machi 24, 2026 wakati wa zinduzi wa kampeni ya kitaifa ya chanjo ya polio ya matone kwa watoto chini ya umri wa miaka 10 akiwa mkoani Mwanza.
"Ili tuweze kuwafikia watoto wengi chanjo hizi zitatolewa kwenye vituo vyetu vya tiba (zahanati, vituo vya afya, hospitali), maeneo mbalimbali ya mukusanyiko (kanisani, msikitini, sokoni, stand ya mabasi na kwenye magulio)," amesema Dkt. Magembe
Dkt. Magembe ametumia fursa hiyo kuwatoa hofu wananchi kuwa chanjo hiyo ni salama kwa matumizi na imethibitishwa na mamlaka za ndani na nje ya nchi.
“Tunatoa chanjo ili kuwakinga watoto wasipate maambukizi ya ugonjwa wa Polio kwa kuwa akishapata mtoto hata mmoja anaweza kuambukiza wengine wengi, hivyo watoto wote wakichanja kinga yao ya mwili itaimarika na kila mtoto atamlinda mwenzie na hatimae jamii yetu yote ya Tanzania itakuwa salama," amesema Dkt. Magembe