BIMA YA AFYA KWA WOTE KUONDOA VIKWAZO KATIKA UPATIKANAJI WA HUDUMA ZA UZAZI
Posted on: February 16th, 2026Na Cletus Sanga, WAF - Katavi
Mfuko wa Bima ya Afya kwa Wote kuondoa vikwazo katika upatikanaji wa huduma za afya ya mama na mtoto kwa kuhakikisha huduma muhimu zinapatikana kwa wakati, usawa na bila kikwazo cha gharama kwa wananchi wote.
Hayo yamebainishwa leo tarehe 16 Februari, 2026 na Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mhe. Mwanamvua Hoza Mrindoko, wakati wa utambulisho wa Mradi wa Mjamzito na Mtoto Salama unaotekelezwa chini ya Shirika la THAMINI UHAI kwa kushirikiana na Wizara ya Afya pamoja na Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, Mkoani humo.
Amesema Serikali imeendelea kufanya jitihada kubwa katika sekta ya afya, ambapo vituo vinavyotoa huduma za afya ya mama na mtoto vimeongezeka kutoka vituo 109 mwaka 2020 hadi vituo 137 mwaka 2025, sawa na ongezeko la asilimia 35.
Aidha, ametoa rai kwa viongozi wa wilaya kusimamia kikamilifu utekelezaji wa mradi huu ili kuhakikisha unatekelezwa kwa ufanisi na kufikia malengo yaliyokusudiwa.
Ameongeza kuwa jitihada za pamoja zinahitajika katika jamii ili kuhakikisha wajawazito wanafika mapema kliniki, pamoja na kuimarisha ushirikiano katika kuwajengea uwezo wataalamu wa sekta ya afya.
Vilevile, Mhe. Mrindoko amesema uhamasishaji kwa jamii unapaswa kuongezwa ili kupunguza idadi ya akina mama wanaojifungulia majumbani.
Kwa upande wake, Mwakilishi kutoka Wizara ya Afya, Joachim Masunga, amesema ni muhimu kuzingatia sera na miongozo ya Serikali katika utekelezaji wa mradi ili kuhakikisha unawanufaisha wananchi ipasavyo.
Pia amewapongeza viongozi wa Mikoa na Halmashauri kwa ushirikiano wanaouonesha katika utekelezaji wa afua za afya ya mama na mtoto.
Ameeleza kuwa Serikali imeendelea kuboresha rasilimali watu katika sekta ya afya, hatua ambayo ni katika maelekezo na juhudi za Samia Suluhu Hassan za kuboresha huduma za afya nchini.
Naye Mkurugenzi wa Shirika la THAMINI UHAI, Bw. Banzi Msumi, amesema kuwa tangu mwaka 2019, Shirika hilo kwa kushirikiana na Wizara ya Afya na TAMISEMI limekuwa likitekeleza ujenzi wa wodi za kujifungulia, ukarabati wa wodi za wazazi kabla na baada ya kujifungua, pamoja na ukarabati wa chumba cha watoto njiti na waliozaliwa na uzito pungufu (KMC) katika Hospitali ya Manispaa ya Mpanda. Pia wamekuwa wakitekeleza Mradi wa Msindikizaji wa Mjamzito katika vituo nane vilivyopo kwenye halmashauri zote tano za Mkoa wa Katavi.
Ameongeza kuwa mradi huu unaenda sambamba na heshima aliyoipata Rais Samia Suluhu Hassan kuchaguliwa kuwa Kinara wa Umoja wa Afrika (AU) wa Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto, ambapo katika kipindi cha mwaka mmoja ataongoza juhudi za kuimarisha mshikamano na hatua za pamoja miongoni mwa nchi wanachama wa AU katika kuboresha afya ya uzazi pamoja na afya ya mama na mtoto barani Afrika.