BIMA YA AFYA KWA WOTE ITAHAKIKISHA WANANCHI WANAPATA HUDUMA ZA AFYA
Posted on: October 4th, 2026Na Aisha Swahibu, WAF, Pwani - Rufiji
Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia masuala ya Dawa na Vifaa Tiba Bw. Emmanuel Tayari amesema Serikali itaendelea kuchukua hatua mbalimbali kuhakikisha utekelezaji wa Bima ya Afya kwa wote unakuwa na tija kwa wananchi.
Bw. Tayari ameyasema hayo leo Oktoba 04, 2026, wakati wa hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa na Chuo cha Afya cha Samia Suluhu Hassan, mkoani Pwani, Wilaya ya Rufiji
Amesema utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote unahitaji ushirikiano wa pamoja kati ya Serikali, Wizara ya Afya na wadau wengine, huku akieleza kuwa Wizara imefanya kazi kubwa katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma za afya kwa wakati na kwa ufanisi.
Bw. Tayari amesema Wizara ya Afya itaendelea kusimamia ujenzi wa Hospitali hiyo mpya ya rufaa na Chuo cha Afya cha Samia Suluhu Hassan vinavyohitajika viweze kukamilika na kuwafikia wananchi kwa urahisi.
Aidha, amesema Wizara ya Afya itaendelea kuimarisha upatikanaji wa dawa na vifaa tiba kupitia Bohari ya Dawa (MSD), ili kuhakikisha Hospitali hiyo havikabiliwi na upungufu wa dawa na vifaa tiba.
Bw. Tayari ameongeza kuwa Serikali inaamini kuwa kupitia Bima ya Afya kwa Wote, wananchi wataweza kupata huduma za afya kwa urahisi zaidi bila vikwazo vya gharama, hivyo kuchangia katika kuboresha afya na ustawi wa jamii.
Amesema uwekezaji unaofanywa na Serikali katika sekta ya afya ni sehemu ya dhamira ya kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora, huku akisisitiza kuwa Serikali itaendelea kuweka rasilimali katika kuimarisha huduma za afya na miundombinu yake.