Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

BILIONI 11.3 ZITATUMIKA KUJENGA MAJENGO MATANO HOSPITALI YA RUFAA YA MKOA SHINYANGA.

Posted on: February 23rd, 2024



Na WAF - SHINYANGA

Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuboresha hali ya utoaji wa huduma za Afya Mkoani Shinyanga kwa kupanga kujenga majengo ya kisasa yenye thamani ya Shillingi Bilioni 11.3 katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa.

Hayo yamesemwa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Grace Magembe wakati wa makabidhiano ya eneo la ujenzi na Mshauri elekezi wa masuala ya ujenzi Katika eneo la Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Shinyanga, zoezi lililoshuhudiwa na Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga Februari 23, 2024.

Ujenzi huo unatarajiwa kuongeza majengo mapya matano ambayo ni jengo la ghorofa tatu la huduma za afya ya mama na mtoto, maabara ya kisasa, jengo la kufulia nguo, jengo la dawa na jengo la
kuhifadhia maiti na hivyo kuo
ngeza wigo wa utoaji wa huduma kwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga.

Katika ziara hiyo, Naibu Katibu Mkuu alikagua ujenzi wa jengo la nje (OPD) ambalo litatoa huduma zote za wagonjwa wa nje ikiwemo upasuaji mdogo. Jengo hilo linalojengwa na Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga litagharimu shilingi milioni 486 na linatarajia kukamilika ifikapo mwezi Machi 31, 2024. Ujenzi wa jengo hilo utapunguza msongamano wa wagonjwa katika kituo cha Afya Kambarage na pia kuboresha huduma za dharura.

Dkt. Magembe ameongeza kuwa kufuatia uwekezaji unaotekelezwa na Serikali katika sekta ya Afya Nchini ni vyema watoa huduma wakasimamia ubora wa huduma wanazotoa ili kuweka tija katika Maendeleo ya Sekta ya Afya.

"Haya maboresho yote yaliyofanyika hayatakuwa na tija endapo watoa huduma za afya hatutabadilika, na kuacha kufanya kazi kwa mazoea, kila mtumishi analazimika kuzingatia weledi ili wananchi wafurahie huduma zinazotolewa" amesema Dkt. Magembe

Pia Dkt Magembe ametoa rai kwa wanaosimamia miradi hiyo ya ujenzi kuhakikisha inakamilika kwa wakati na kuanza kutumika ili wananchi wafaidike na uwekezaji unaofanywa na serikali yao katika sekta ya afya.