BARAZA LIFAHAMU MTAZAMO WA WADAU JUU YA WATAALAMU WA TIBA ASILI-BALOZI KASHERA
Posted on: October 20th, 2026Na WAF-Dar es Salaam
Mtaalamu wa Itifaki Balozi Omary Kashera Mjenga amesema ili sekta ya tiba asili na tiba mbadala iweze kupata mafanikio na kupiga hatua kubwa nchini, ni muhimu kufahamu na kuzingatia mtazamo wa wadau mbalimbali pamoja na jamii kwa ujumla kuhusu wataalamu wanaotoa huduma hizo.
Balozi Kashera ametoa msisitizo huo katika kikao cha siku mbili cha Baraza la Tiba Asili kilichofanyika Oktoba 19 na 20 Jijini Dar es Salaam kwa lengo la kufanya tathmini ya utoaji wa huduma za tiba asili.
“Baraza kuwa na uelewa juu ya mtazamo wa wadau muhimu mnaoshirikiana nao, kwani kujua mtazamo wao kwenu kutawafanya kupata namna bora ya kushirikiana nao pindi mnapohitajiana na kuleta matokeo chanya,” amesema Balozi Kashera.
Katika kikao hicho, Balozi Kashera ameeleza kuwa, kutambua mtazamo wa wadau ni hatua ya msingi katika kujenga uaminifu, kuondoa dhana potofu na kuleta mabadiliko chanya katika sekta ya tiba asili na tiba mbadala nchini.
Amesisitiza kuwa uelewa huo utasaidia Baraza kuweka viwango bora vya utendaji kazi na kuwawezesha wataalamu wa tiba asili na tiba mbadala kutoa huduma zenye ubora unaokubalika.
Aidha, amebainisha kuwa na mtazamo chanya kutoka kwa wadau ni chachu ya kuimarisha utambuzi rasmi wa wataalamu wa tiba asili na tiba mbadala pamoja na ushirikiano wao na Wizara ya Afya, hatua inayolenga kuwezesha maendeleo ya sekta hiyo nchini.