APOTHEKER YAONGEZA NGUVU KATIKA TEHAMA YA WIZARA YA AFYA
Posted on: June 11th, 2025
Na, WAF-Dodoma
Wizara ya Afya imepokea vifaa vya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kutoka kwa shirika lisilo la kiserikali la Apotheker Health Access Initiative, ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za serikali katika kuimarisha mifumo ya kidijitali kwenye sekta ya afya nchini.
Makabidhiano hayo yamefanyika leo Juni 11, 2025 na kuhudhuriwa na Mkurugenzi wa TEHAMA wa Wizara ya Afya, Bw. Silvanus Ilomo, aliyepokea vifaa hivyo kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dkt. Seif Shekalaghe. Vifaa vilivyokabidhiwa ni pamoja na kompyuta mbili, printer, projector pamoja na samani za ofisi ambavyo vitasaidia kuongeza ufanisi wa kazi na kuimarisha matumizi ya mifumo ya kidijitali.
Akizungumza katika hafla hiyo, Bw. Ilomo ameishukuru Apotheker kwa mchango wao muhimu unaolenga kuimarisha sekta ya afya kupitia TEHAMA. “Tunatambua na kuthamini mchango wenu katika kusaidia utekelezaji wa dira ya Wizara kuwa na huduma za afya zilizo kidijitali, bora na zinazowafikia wananchi kwa urahisi,” amesema Bw. Ilomo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mipango na Uendeshaji wa Apotheker Dkt. Angel Dillip, amesema kuwa wao kama wadau wa Serikali wataendelea kushirikiana na Wizara katika kuhakikisha azma ya kufanikisha huduma za afya kwa njia ya kidijitali inatimia.
Aidha Dkt. Angel amesisitiza kuwa huduma bora za afya zinahitaji ushirikiano wa pande tatu, mtoa huduma, mpokeaji wa huduma, na mtu wa kati anayerahisisha mawasiliano na upatikanaji wa taarifa.
Apotheker Health Access Initiative ni shirika linalojihusisha na utafiti, mafunzo na utoaji wa huduma za afya, likiwa na dhamira ya kuboresha ustawi wa jamii kupitia ubunifu, ushirikiano na ubora katika sekta ya afya.