Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

ALIYETESEKA NA TATIZO LA KUOZA SEHEMU YA UTUMBO, MADAKTARI BINGWA WA SAMIA WAMREJESHEA FURAHA

Posted on: June 3rd, 2025

Na WAF, MANYARA


Madaktari Bingwa wa Rais Samia wamefanikiwa kumfanyia upasuaji wa utumbo mwanaume mmoja mwenye umri wa miaka (69) ambaye jina limehifadhiwa aliyeteseka na tatizo hilo kwa zaidi ya miazi sita.


Hali hiyo imebainika Juni 04, 2025  ambapo mwananchi huyo alifika Hospitalini hapo akiwa na maumivu makali na kushindwa kufanya shughuli za maendeleo. 


Kwa mujibu wa Madaktari Bingwa hao walibaini sehemu ya utumbo mpana ikiwa imejikunja kwa nyuzi 720, hali iliyosababisha utumbo huo kujaa na kuharibika na kuonyesha dalili za utumbo kuoza.


"Aliletwa jana hapa tukamfanyia vipimo na tukabaini utumbo mpana ulikuwa umejifunga, tukamuandaa kwa ajili ya upasuaji, wakati wa upasuaji tumekuta utumbo umejikunja zaidi ya mara mbili, umejaa na kuoza ikabidi tukate sehemu ya utumbo uliooza na hadi sasa mgonjwa anaendelea vizuri" amesema Dkt Julius Mollel, Daktari Bingwa wa usauaji.


Hapo awali mgonjwa huyo, aligunduliwa kuwa na tatizo la tumbo (acute abdomen) takribani wiki mbili zilizopita na akaelekezwa kupata huduma ya kibingwa katika ngazi ya juu, hata hivyo, kutokana na changamoto za kifedha, hakuweza kufanikisha rufaa hiyo na hivyo kulazimika kurejea nyumbani.


Mara baada yakupata taarifa za ujio wa madaktari Bingwa mgonjwa huyo alifika hospitalini hapo kufanyiwa uchunguzi wa kitaalamu na vipimo vya picha vilivyobaini kujikunja kwa sehemu ya utumbo mpana kisha kufanyiwa upasuaji huo. 


Bi Fatuma Hamis na Bi Jamila Issa ambao ni wake wa mgonjwa huyo, pamoja na mtoto wake Ramadhan Mzamiru wametoa shukrani kwa Madaktari hao na kwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuanzisha mpango huo wa madaktari bingwa kwani umeokoa maisha ya Mzee huyo.


"Kusema kweli hatukutegemea kama angeweza kuendelea vizuri hivi kwa hali aliyokuwa nayo awali, Tunashukuru sana Mama (Rais Samia) kwa kututumia hawa madaktari tunamuombea Mungu azidi kumbariki katika uongozi wake" ameeleza Jamila Issa, Mke wa Mzee huyo.


“Hatuna cha kulipa zaidi ya kusema ahsante sana kwa madaktari hawa, kama siyo kambi hii ya Rais Samia, baba yetu huenda angelipoteza maisha kutokana na changamoto ya kifedha tuliyonayo, huduma hii ni msaada mkubwa kwa sisi wa kipato cha chini”. amesema mtoto wa Mzee huyo.


Upasuaji huo umefanywa na Daktari bingwa wa Upasuaji Dkt. Julius Mollel, Daktari Bingwa wa dawa za usingizi na ganzi tiba salama Dkt.Anna Dohho, Muuguzi bingwa wa Upasuaji Emelda Obara pamoja na timu nyingine ya madaktari wa hospitali hiyo.


Huduma za kibingwa katika Mkoa wa Manyara zinaendelea kutolewa katika Hospitali za Halmashauri za mkoa huo hadi Juni 07, 2025 katika Hospitali ya Wilaya ya Tumaini, Hospitali ya Wilaya ya Kiteto (Kibaya), Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Babati Mjini, Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Babati Vijijini, Hospitali za Halmashauri ya Mbulu na Mbulu Mjini, Hospitali ya Wilaya ya Simanjiro.