Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima

 

 

Na Emmanuel Malegi – Dodoma

Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kupitia Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) kwa kushirikiana na Baraza la Famasi, Baraza la Mifugo TAMISEMI Pamoja na jeshi la Polisi imefanya operesheni maalum kati ya Tarehe 15 na 20 Machi 2021 na kubaini Dawa, Vifaa tiba na vitendanishi bandia, duni na ambazo hazijasajiliwa na TMDA katika baadhi ya mikoa nchini.

Hayo yamebainishwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima mapema leo mbele ya waandishi wa Habari na kuongeza kuwa operesheni hiyo Pamoja na mambo mengine ilikua na lengo la kubaini uwepo wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi vya Serikali vinavyouzwa katika maduka na vituo binafsi.

Dkt. Gwajima amesema katika operesheni hiyo pia wataalamu wameweza kubaini uwepo wa dawa zilizoisha muda wa matumizi na zile ambazo zimeghushiwa ili kuonesha zinafaa kwa matumizi.

“Jumla ya majengo 905 yalikaguliwa ambapo kati yake 334 ni famasi, 28 ni maduka ya vifaa tiba, 21 ni maghala ya dawa, 11 maghala ya vifaa tiba, 115 maduka ya dawa za mifugo, 329 maduka ya dawa muhimu za binadamu, 29 vituo vya kutolea huduma za afya, 28 maabara na kiwanda kimoja cha dawa”. Amesema Dkt. Gwajima.

Katika operesheni hiyo dawa bandia aina tatu zilibainika zenye thamani ya Shilingi 857,000 ambazo ni Alben Blue ambayo uchunguzi uliofanywa na TMDA umethibitisha dawa hii haina kiambata hai, Gentrosone Cream ambayo imebainika haina viambata hai vya Clotrimazole, Gentamicin Sulphate na Betamethasone Diproprionate Pamoja na dawa Benzathine Penicillin injection ambayo imebainika kuwa tarehe za kutengenezwa na kuisha muda wa matumizi zimeghushiwa.

Aidha, Dkt. Gwajima amesema dawa za Serikali zenye thamani inayokadiriwa kufikia Shilingi 691,000 zilikutwa zinauzwa katika maduka ya dawa na vituo vya afya binafsi.

Waziri amebainisha kuwa vifaa tiba na Vitendanishi vya Serikali vinavyokadiriwa kuwa na thamani ya Shilingi Milioni Tano vilikamatwa katika vituo na maduka binafsi ambavyo vilikua na maandishi ya “For GOV-TZ NOT FOR SALE”.

Waziri Gwajima amesema wizi wa bidhaa za afya za Serikali kwenda nje ya mfumo wa Serikali ni mkubwa na Wizara kupitia taasisi zake na wadau wanafuatilia mnyororo wa wizi na hatua zaidi zitafuata ikiwemo kuwafikisha mahakamani sambamba na kuwapeleka mbele ya mabaraza na bodi za kitaaluma kwa ajili ya kuchukua hatua kali.

Hata hivyo, Waziri Gwajima amesema jumla ya Shilingi Milioni 86.38 zimekusanywa kama faini kwa wale ambao makosa yao hayakuhitaji kuwafikisha mahakamani ambapo faini hizi ni gharama za utekelezaji aslimia 25 na tozo ya kukwepa kulipia gharama za uingizaji bidhaa nchini asilimia 2.

Kufuatia hatua hiyo, Waziri Gwajima amelielekeza Baraza la Famasi nchini kusimamisha au kuwafutia usajili kwa mujibu wa kifungu Na. 45 (1) cha Sheria ya Famasi Sura 311 ikiwemo kuwachukulia hatua wamiliki wa maduka na maeneo ya biashara wanaokiuka taratibu na kanuni za uendeshaji.

Waziri Gwajima ametoa wito kwa wale wanaojihusisha na utengenezaji, usambazaji na uuzaji wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi kuacha mara moja kwaani kuendelea kufanya hivyo ni kielelezo kuwa wameshindwa kutoa huduma inayoleta afya bali wanatoa huduma inayoleta magonjwa, ulemavu na vifo kwa makusudi na kinyume na Sheria ya Dawa na Vifaa Tiba, Sura 219 pamoja na sheria nyingine za nchi.

Feature News & Events

Go to top